"Elimika, Elimisha, Burudisha"

 1. Yose Hoza
 2. Kiswahili
 3. Alhamisi, 25 Januari 2018
KITABU CHA KUSADIKIKA

MASHTAKA
Waziri wa Kusadikika alikuwa mtu mwenye haiba kubwa na uhodari mwingi. Kwa hivi aliitwa Majivuno.

Uwaziri wake ulianza zamani sana. Alikuwa Waziri wa wafalme watatu katika nyakati mbalimbali.

Babu yake mfalme anayesimuliwa aliposhika ufalme, yeye alishika uwaziri; baba yake aliposhika unahodha wa chombo cha serikali, yeye alikuwa rubani wake; akaendelea katika hadhi hiyo mpaka wakati wa enzi ya mfalme mpya.

Umri wake mkubwa ulizifanya nywele zake kichwani kuwa nyeupe. Kwa haiba hii aliweza kufanyiza kuyavuta macho ya watu; na kwa ufasaha wa maneno aliweza kufanyiza fungu au mwamba wa kuyavunja maisha ya mtu yeyote kama chombo.

Kipawa chochote cha mtu kama hakikuongozwa vema huweza kuwa hatari au maangamizi kwa wengine. Mtu huyu alikuwa maarufu na mashuhuri lakini alijaa tadi na inda kama hadithi hii inavyosimulia.

Majivuno aliyaanza mashitaka yake kwa kusema, "Jalali Mfalme na madiwani wakuu wa baraza.

Nataka kuweka mbele yenu mashitaka ya serikali ya Kusadikika juu ya Karama, raia mmoja, anayelindwa na ulinzi wa mfalme, lakini si mwaminifu; anayefaidi haki na mapendeleo ya utawala huu, lakini hana shukrani; na aliye chini ya bendera ya nchi hii, lakini si mtii.

Miaka kumi imepita tangu mnong'ono wa kwanza ulipofika katika sikio langu kuwa mshtakiwa alikuwa mtu mwenye bughudha nyingi juu ya taratibu za utawala wa Kusadikika, na hasa juu ya hukumu zilizotolewa na mahakimu katika baraza.

Ilisemwa kuwa mshitakiwa alidai kuwa hukumu chache sana zilikuwa za haki, lakini nyingi zilikuwa za dhuluma tupu. Kwanza mimi sikufikiri kamwe kuwa hili liliweza kutoka katika kinywa chake, na hata kama lingaliwezakana niliona kuwa tone moja la maji haliwezi kuleta gharika katika nchi."

"Baadaye mnong'ono uleule wa kwanza ulikaririwa katika sikio langu. Lakini sasa niliambiwa kuwa mshtakiwa alikuwa kiongozi mwenye wafuasi wengi waliokuwa wakijifunza uanasheria chini yake.

Ukariri huu ulinishitua sana. Niliona kama radi imenipasukia ghafla bila ya kufanya wingu ingawa nilikumbuka waziwazi kuwa habari za mshitakiwa nilikwisha zisikia zamani.

Tone dogo la maji, lile nililodhania kuwa litakauka lenyewe mara moja, limekuwa mlizamu wa kuwafariji kwa siri wanafunzi wa mshtakiwa.

Upelelezi huo ulidhihirisha bila ya shaka yoyote kuwa mshtakiwa alikuwa akiwafunza watu watu, siyo kuomba msamaha na huruma katika baraza tu, lakini hata kuzibatilisha hukumu za baraza la Kusadikika kwa njia zote.

Hili lilionyesha kuwa mgogoro mkubwa sana utakuwako kati ya sheria za nchi na watu wake."

"Ilipoonekana kuwa matendo ya mshtakiwa yalikuwa hayavumiliki, na yenye hatari kubwa kabisa katika nchin, niliamuru akamatwe na kuhukumiwa.

Alipofika mbele yangu mara ya kwanza aliulizwa kama alikuwa mwalimu wa wanasheria. Alikubali upesi kama aliyeona ametunukiwa hadhi kubwa.

Wa aidha alisema kuwa nafasi ya mwanasheria katika nchi hii alikuwa tupu. Kwa hivi alikusudia kuwa mwanasheria wa kwanza wa Kusadikika.

Nilimwambia kuwa wakati ulikuwa umewadia wa kukoma kujidanganya yeye mwenyewe na watu wengine tena kwa matumaini ya kuwa mwana hivi au mwana vile bila idhini ya serikali."

"Nataka ifahamike waziwazi kuwa nina hofu kubwa sana juu ya mshtakiwa. Sababu za hofu yangu ni kuwa kama akiamriwa kuwa kama atakavyo leo, kesho atadai udiwani, kesho kutwa uwaziri, na baadaye ufalme.

Kwa desturi, tamaa za watu kama yeye alivyozitamka. Tamaa hizo zikiamka hazitokuwa na mipaka. Watu kama hao lazima wafunzwe kuzijua hali zao zilivyo katika maisha, na mwisho wa tamaa zao vilevile."

"Matendo ya mshtakiwa yalipasa kukomeshwa wakati yalipoanza. Walakini kwa sababu ya tabia yangu njema, na saburi ambayo kila waziri kuwa nayo, mashitaka haya sikuyaleta barazani mpaka leo.

Nilidhani kuwa mshiltakiwa akiona kuwa bidii yake ilikuwa kazi bure, atakoma mwenyewe kuyadhihaki mamlaka ya serikali

Badala ya kusoma, alijiona amepata nafasi ya kuyaeneza bila ya ruhusa ya serikali mafunzo yake yasiyotakiwa katika nchi ya Kusadikika."

KWA UFUNDI HUO WA WAZIRI MAJIVUNO KATIKA UWASILISHAJI HOJA, BWANA KARAMA ATAPONA KWELI MBELE YA MFALME? ...
Maoni
Hakuna maoni kwa sasa.


Hakuna maoni yoyote kwa sasa. Kuwa wa kwanza kutoa maoni yako!
Guest
Wasilisha Maoni Yako
Sakinisha faili au picha kwenye mjadala huu kwa kubonyeza kitufe cha sakinisha hapa chini. Inapokea gif,jpg,png,jpeg,zip,rar,pdf
• Insert • Futa Sakinisha faili (Lisizidi ukubwa wa: 2 MB
Weka Eneo Ulipo

Kuweka eneo ulilopo wakati wa kutoa maoni yako inawezesha wajumbe kujua mahali ulipo.

Latitude:
Longitude:

Jukwaa la Elimika

Mijadala

Afya
 1. Mijadala 6
 2. MIjadala midogo
Kiswahili
 1. Mijadala 20
 2. MIjadala midogo
Michezo
 1. 1 post
 2. MIjadala midogo
Teknolojia
 1. Mijadala 8
 2. MIjadala midogo
Mchanganyiko
 1. Mijadala 18
 2. MIjadala midogo

WASILIANA NASI

Elimika, Ghana Avenue, Posta House
SLP: 73622 Dar Es Salaam, Tanzania
Simu: 0764 006 222
Barua Pepe: info@elimika.co.tz

UNGANA NASI

VIGEZO NA MASHARTI

Ni haki yako kuzifanya taarifa zako kuwa za siri, hivyo basi, taarifa zako ni siri yako na hazitasambazwa popote ila zile zilizo upenuni, zitatumika kwaajili ya maendeleo ya jukwaa hili. Soma Zaidi

©2018 Elimika. Haki Zote Zimehifadhiwa. Imeundwa na SphereCom.

Search